Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wahudumu wa mabasi ya usafiri Mombasa wameitaka idara ya usafiri nchini kufanya uchunguzi na kuwakamata baadhi ya watu wanaofanya biashara hiyo kwa kutumia magari ya kibinafsi kinyume cha sheria.

 

Wahudumu hao wanasema uchunguzi wao umebaini kuna baadhi ya watu wanaotumia magari madogo ya kibinafsi ambayo hayajasajiliwa rasmi na kubeba abiria kwa bei nafuu jambo linaloleta changamoto katika biashara hiyo.

 

Akiongea na mwandishi huyu katika kituo cha mabasi cha Mwembe tayari siku ya Jumanne, mhudumu mmoja kwa jina Edwin Nzuve alisema watu hao wamekuwa wakitumia ujanja kukwepa vituo vya trafiki barabarani.

“Hizo ni zile gari ndogo za kibinafsi, unajua ni vigumu kuwatambua kwa sababu polisi watadhani ni mtu amebeba familia yake wakisafiri kumbe ni biashara wanafanya,” Nzuve alisema.

Wanasema hali hiyo imeathiri pakubwa biashara yao kwani abiria wengi hukimbilia gari hizo ndogo ambazo hubeba abiria kwa bei ya chini na kufanya biashara ya usafiri wa mabasi kudorora.

Wameitaka mamlaka ya usafiri nchini NTSA kuchunguza swala hilo na kusema kuwa wana ushahidi kuthibitisha visa hivyo ambavyo hutokea mara kwa mara katika barabara kuu ya Mombasa Nairobi.