Kinara wa Cord Raila Odinga ameeleza kuwa ana imani kuwa mrengo huo ungali maarufu katika eneo la Pwani, licha ya baadhi ya wanasiasa waliochaguliwa kwa tiketi ya Cord kutangaza kuhama na kujiunga na upinzani.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Odinga alisema kuwa mrengo huo hauwezi yumbishwa na siasa za Jubilee na kuwa utazidi kupata uungwaji mkono kutoka kwa wakaazi.
Raila alimkosoa Rais Uhuru Kenyatta kwa kudai kuwa alitumia ziara yake mjini humo kujipigia debe kisiasa, badala ya kuitekeleza miradi ya maendeleo kwa wenyeji.
Katika hotuba yake kwa wakaazi, Odinga pia alimkosoa Seneta wa Nairobi Mike Sonko, kwa kile alichokitaja kama kuwakosea heshima viongozi wa Mombasa, kufuatia matamshi aliyoyatoa katika halfa ya kutoa hati miliki kwa maskwota wa shamba la Waitiki mapema mwezi huu.
“Juzi Sonko alikuja hapa na kumtusi gavana wetu mbele ya rais na hakuchukuliwa hatua yoyote. Hatutaki viongozi wasiowaheshimu wenzao,” alisema Odinga.
Aidha, kiongozi huyo wa upinzani alisema ana imani kuwa chama cha ODM kitazoa ushindi katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi, ambao umeratibiwa kufanyika Machi 7, 2016.
Odinga vilevile aliwahimiza vijana wa Pwani kuwa wastahimilivu na kujituma katika maisha yao ya kila siku, huku akiwaahidi kuwa mambo yatabadilika iwapo atashinda katika uchaguzi wa 2017.