Gavana James Ongwae amewaomba maafisa katika Kaunti ya Kisii kushirikiana kuwasaidia vijana kujiendeleza kimaisha.
Ongwae alisema kuna haja ya vijana katika Kaunti ya Kisii kusaidiwa na maafisa hao, ili kujiunga na vikundi mbalimbali vitakavyo wawezesha kuwekeza pesa kwa matumizi ya siku za usoni.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Kisii wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusafisha mji huo na kupambana na mikasa itakayoletwa na mvua ya El Nino, Ongwae alisema vijana wanastahili kujiunga na vikundi na kusaidiwa na maafisa wa kaunti ili kujiendeleza kimaisha.
“Naomba maafisa wangu tusaidie hawa vijana ili waanze kuwekeza baada ya kujiunga na vikundi ili waweze kujiimarisha kimaisha,” alisema Ongwae.
Gavana Ongwae alisema iwapo umaskini utapunguzwa katika Kaunti ya Kisii haswa miongoni mwa vijana, sharti wasaidiwe katika kujiendeleza.
“Umaskini utapungua katika kaunti yetu tukishirikiana pamoja kwa kufanya biashara na kilimo ili tuinue uchumi wa taifa,” alisema Ongwae.
Ongwae aliwaomba viongozi wa Kaunti ya Kisii kuweka siasa kando na kuwatumikia wananchi kwa kufanya maendeleo, huku akisema wakati huu si wakati wa siasa ila ni wakati wa kuleta maendeleo kwa kufanya waliyowahidi wakazi wakati wa kampeini.