Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kijamii la ‘Kenya Community Support Centre’ Phyllis Muema amewataka maafisa wa polisi kuzingatia ripoti wanazopewa na vijana za kihalifu ili kuzuia kuchipuka kwa makundi ya kihalifu.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne baada ya kuhudhuria kongamano la vijana kuhusu uhamasisho, Muema alisema kuwa kutokana na wengi wa vijana kujinasua katika makongamano ya hamasa kwa kiasi kikubwa kumepunguza visa vya kihalifu, hivyo basi itakuwa vyema iwapo polisi watawajibika.
Alihimiza vijana na jamii kwa jumla kushirikiana kwa karibu mno na maafisa wa polisi ili kukomesha uhalifu sambamba na kuimarisha usalama wa eneo zima la Pwani.
"Tunawaomba maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa wanazingatia ripoti za kihalifu wanazopewa na jamii pamoja na vijana ili kuona kuwa usalama unaimarishwa na kukabiliana vyema na makundi ya kihalifu, na vijana pia tunawahimiza kushirikiana na maafisa wa polisi kwa karibu mno ili kuwakabilia wahalifu," alisema Muema.
Mwanaharakati huyo wa kijamii alisema kuwa wameandaa mikakati inayowahusisha moja kwa moja maafisa wa polisi na vijana katika juhudi za kudumisha usalama kupitia mtandao wa kijamii.