Serikali ya kaunti ya Nakuru imetakiwa kununua magari zaidi ya kuzima moto ili kukabiliana na mikasa inayotokea mara kwa mara.
Wito huo umetolewa na wakaazi wa kaunti ya Nakuru haswa eneo bunge la Bahati, ambapo wikendi iliyopita mikasa miwili ya moto ilitokea.
Wakaazi walidai gari la kuzima moto kutoka makao makuu ya kaunti likachelewa kufika.
Kulingana na wenyeji hao waliozungumza na mwandishi huyu Jumanne, walisema ingekuwa rahisi kupigana na majanga ya moto yanayotokea katika baadhi ya kaunti ndogo kama vile Bahati, Molo, Elburgon na Mai Mahiu iwapo watapata zima moto zaidi.
Mkaazi James Mburu alisema: “Serikali yetu ya kaunti iongeze zima moto katika kila eneo bunge kwa sababu gari lililopo linachukua muda mrefu kufika katika eneo la mkasa."
Catherine Ngoiri, alipendekeza wananchi wapewe mafunzo zaidi kuhusiana na matumizi bora ya umeme, gesi na jinsi ya kuepuka mikasa inapotokea.
“Wakati moto ulitokea hapa Jumamosi, watu wengi walifurika hapo hata ikawa vigumu kwa walio na uwezo wa kukabiliana na moto kuuzima. Tungekuwa na vijana waliopewa mafunzo ya kupigana na majanga kama haya, ingekuwa bora zaidi,” Ngoiri alisema.