Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua ameelezea kuwa serikali yake iko tayari kusaidia vijana kuimarisha viwango vyao vya elimu ili kuwapa ujuzi utakaowasaidia kujikimu maishani.

Mbugua kwa ushirikiano na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Bonde la Ufa ameelezea kuwa serikali yake itaboresha viwango vya mafunzo katika vyuo vya kiufundi vilivyoko kwenye kaunti hiyo ili vijana wapate maarifa ya kutosha.

"Lengo letu ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na maarifa ambayo yatawafaa maishani ili wapate kujikimu," alisema Mbugua.

"Kwa ushirikiano na taasisi hii, tutahakikisha kuwa viwango vya mafunzo vimeimarishwa katika kila chuo," aliongeza Mbugua.

Gavana huyo alisema hayo wakati wa mkutano wake na mkuu wa taasisi hiyo Eddy Koimett miongoni mwa viongozi wengine serikalini. 

Koimett kwa upande wake amemshukuru Mbugua kwa jitihada zake katika kuwasaidia vijana wa eneo hilo kupata elimu na ujuzi wa kiufundi.

"Tunafurahia sana juhudi za serikali ya Nakuru za kuwasaidia vijana ili kupata elimu na ujuzi mbalimbali ili wapate kujitegemea maishani," alisema Koimett.

"Tutakuwa imara kuungana na serikali katika mradi wowote ule ambao utanuia kuimarisha viwango vya elimu kwa vijana," aliongeza Koimett.

Koimett pia alichukua fursa hiyo kupongeza mradi wa Gavana Mtaani ambao umechangia pakubwa kuimarisha maisha ya wengi katika eneo hilo.

"Huduma ambazo kaunti hii imetoa kwa wananchi kupitia mradi wa Gavana Mtaani umechangia pakubwa kusaidia watu kupata huduma hizo kwa urahisi na mwishowe kufaidika," alisema Koimett.

"Hili linaonyesha kuwa serikali hii iko imara kutimiza ahadi yake kwa wananchi," aliongezea Koimett.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo ni naibu gavana Joseph Ruto na waziri wa elimu wa kaunti hiyo Francis Methea.