Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Muhuri, sasa linaitaka serikali kuwaondoa wanajeshi wa Kenya KDF nchini Somalia ili kuimarisha usalama wa nchi.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hassan Abdille amesema kuwa hatua iliyochukua serikali kuwapeleka wanajeshi wa Kenya nchini Somalia chini ya uongozi wa Shirika la wanajeshi wa kimataifa Amisom kamwe haukuwa uamuzi bora.
Akiongea na wanahabari katika afisi za shirika hilo mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Abdille alisema kuwa kama shirika watahakikisha kuwa wameishinikiza serikali na kuwaondoa wanajeshi hao nchini humo na akaitaka serikali kubuni mbinu mbadala za kushirikiana na Amisom.
“Tunaitaka serikali kuwaondoa wanajeshi wetu wa KDF Somalia kwani kuzidi kusilia nchini humu ni tishio la usalama wetu na tunaitaka serikali kulifikiria suala hilo kwa haraka, sisi tumechoka kuona wanajeshi wetu na wananchi wakiuwawa kiholela,” alieza Abdille.
Alisema kuwa kuendelea kuwepo kwa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia kunazidi kutia wananchi hofu ya kiusalama kwani taifa hili bado halijaimarika kiusalama.
Mwanaharakati huyo amependekeza serikali kuwalipa fidia familia za wanajeshi waliyouwawa katika shambulizo hilo lililotekezwa na wanamgambo wa Alshabab katika kambi ya jeshi la KDF eneo la El Adde nchini Somalia.