Shirika la Muhuri lenye makao yake mjini Mombasa limepinga hatua ya serikali ya kupeleka majeshi ya KDF nchini Somalia, kupambana na kundi la al-Shabab.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu lilisema kuwa serikali haikufanya mashauriano kikamilifu na mashirika mbalimbali ya hapa nchini, hatua iliyosema kuwa imesababisha madhara ambayo taifa hili linapitia kutoka kwa kundi hilo.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Hassan Abdille alisema kuwa serikali ya Kenya inafaa kuondoa jeshi hilo nchini humo.
“Bado hatujachelewa. Serikali inafaa kufikiria mara mbili na ikiwezekana iwaondoe wanajeshi hao nchini Somalia. Tunaamini kwamba tukifanya hivyo taifa letu litakuwa salama,” alisema Abdille.
Aidha, Abdille alisema mashambulizi ambayo yamekuwa yakifanywa humu nchini na kundi hilo ni njia moja ya kundi hilo kulipiza kisasi.
Alisema kwamba serikali itakapowaondoa wanajeshi hao Somalia, visa vya uvamizi hapa nchini vitakoma.
Wakati huo huo, shirika hilo limeitaka serikali kufidia familia za wanajeshi waliopoteza maisha wakati wa shambulizi la siku ya Ijumaa, katika kambi yao nchini Somalia.
“Kuna haja ya kuwalipa fidia wale watu ambao wapendwa wao walipoteza maisha katika vita hivyo. Serikali ikae chini ipange mikakati kwa sababu hawa ni Wakenya ambao walijitolea maisha yao kwa ajili ya taifa,” aliongeza mkurugenzi huyo.
Kumekuwa na hisia mbalimbali nchini tangu serikali kupeleka wanajeshi wa KDF nchini Somalia kupambana na kundi la kigaidi la al-Shabab.
Kuna wale wanaounga mkono hatua hiyo wakisema itasaidia kusambaratisha kundi hilo, huku wengine ikiwa ni pamoja na upande wa upinzani wakipinga vikali hatua hiyo, kwa madai kwamba inachochea zaidi mashambulizi ya ndani ya nchi.
Muda mfupi baada ya shambulizi la Ijumaa, Rais Uhuru Kenyatta akihutubu kutoka mjini Mombasa alitoa risala za rambirambi kwa familia za wanajeshi hao na kusisitiza kuwa hata baada ya uvamizi huo, bado serikali itaendelea na mapambano nchini Somali, na kwamba haiko tayari kuondoa jeshi lake eneo hilo.