Huku uchaguzi wa eneo bunge la malindi ukitarajiwa kufanywa hii leo, wenyeji kutoka maeneo ya Pwani wamesema kuwa hawatashawishika kwa njia yoyote ile kuchagua mtu kwa sababu ya chama bali kwa maazimio ya mgombeaji husika.
Wakiongea na mwandishi habari huyu katika eneo bunge la Malindi siku ya Jumapili, wakazi hao walisema kuwa wanasiasa kazi yao imekuwa kujaribu kuwapotosha kuchagua mtu ambaye wenyewe hawajampendelea, hali ambayo mara nyingi huleta ukinzani hasa katika masuala ya maendeleo kwa sababu ya kumpigia mtu kura kwa sababu ya kiongozi wa nchi au ushawishi wa gavana flani.
Jaspher Murima, ambaye ni mwanaharakati wa vijana na kura katika katika eneo hilo aliwataka vijana kuamka kutoka kasumba za zamani na kuanza kufanya uamuzi wao bila kuvutwa na nguvu za viongozi wa kisiasa.
Murima, ambaye alikuwa kwenye harakati za kuwahamasisha vijana dhidi ya kupiga kura na kufanya uamuzi binafsi alisema kuwa baadhi ya vijana wameapa kuzingatia maono na maazimio ya wagombeaji, japokuwa alisema wengi wao hujipata kwenye majaribu ya kushawishiwa kwa pesa ikizingatiwa kuwa wengi hawana kazi.
“Vijana wengi watapiga kura kwenye mrengo pinzani kwa sababu wengi wao hawana kazi, hivyo ni rahisi kununuliwa na wanasiasa na kupiga kura upande ambao hawapendelei,” alisema.