Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali imesema itatoa maelekezo na sera za kukabiliana na ukabila hasi katika taasisi za masomo ya juu, waziri wa elimu Fred Matiang'i amesema.

Alisema kwamba kumekuwa na ongezeko la visa vya watu kuteuliwa ama kupandishwa vyeo kulingana na ukabila katika vyuo vikuu hapa nchini.

Akiongea hapa Nakuru Ijumaa wakati wa kufunga kongamano la siku tatu la masomo ya vyuo vikuu, waziri huyo alisema kwamba uteuzi wowote ule ni lazima uongozwe na kuhitimu kwa mtu na kuna haja kubwa ya swala hilo kupewa uzito mkubwa.

“Viongozi wa Kenya ni lazima waache kusimamia vyuo vikuu kwa kuzingatia matakwa ya kikabila na zawadi za kisiasa. Kuteua watu katika misingi ya kufaulu itasaidia kukabiliana na ukabila,” alisema Matiang’i.

Aliongeza kwamba ukabila na maendeleo ya vyuo vikuu umehatarisha uongozi.

“Wahadhiri wakuu, manaibu wao na watala wengine huteuliwa kutoka kwa wale ambao wanazunguka chuo hicho. Hii inamaanisha kwamba teuzi zinafanywa kulingana na matakwa ya kikabila, mara nyingine pasi na kuzingatia kuhitimu kwa mtu kushikilia nyadhifa hiyo,” alisema.