Share news tips with us here at Hivisasa

Vijana katika eneo la Pwani wamehinzwa kujitenga na masuala ya uhalifu, na badala yake kijihusisha katika michezo ili kutimiza malengo yao katika siku za usoni.

Kulingana na Afisa wa masuala ya sheria na haki katika shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Haki Afrika Francis Auma, idadi kubwa ya vijana wamejiunga na uhalifu kutokana na ukosefu wa ushauri kutoka kwa viongozi wa tabaka mbalimbali katika eneo la Pwani.

Akizungumza mjini Mombasa katika mkutano wa vijana siku ya Ijumaa, Auma amesema kuwa ni jukumu la kila kiongozi, wazazi na jamii kwa jumla kujitokeza kikamilifu na kuwashauri vijana kujikinga na baadhi ya watu flani walio na malengo potovu ya kuwatumia vibaya na kutekeleza uhalifu.

Auma amesema kuwa kama shirika wameandaa michezo mbalimbali ya kuwahusisha vijana na kuwaondoa maskani ili kuona kuwa masuala ya uhalifu na utumizi wa mihadarati kwa kiasi kikubwa inapungua na eneo la Pwani linabaki salama.

“Tumeanzisha michezo mbalimbali ya kuwajumuisha vijana na kuhakikisha kuwa wameondoka maskani na kujiunga na michezo tunayoifanya ili kuhakikisha kuwa eneo hilo halina tena wahalifu wala watumizi wa mihadarati,” alieleza Auma.

Shirika hilo la Haki Afrika lililo na makao yake mjini Mombasa limeandaa michezo hiyo kuhakikisha kuwa vijana wanajitenga na maovu ikiwemo uhalifu, mihadarati na ubakaji.