Viongozi kutoka Pwani walioasi mrengo wa Cord wameapa kuendelea kushirikiana na chama cha JAP licha ya vitisho kutoka kwa chama cha upinzani kuwa watafanya kampeni za kuhakikisha kuwa wanapoteza viti vyao vya ubunge.
Gideon Mung’aro wa Kilifi Kaskazini na mwenzake Mustafa Iddi kutoka eneo bunge la Kilifi Kusini walisema kuwa hawatatishwa na vitisho vyovyote vinavyotolewa na muungano wa Cord, na kusisitiza kuwa wataendelea kumfanyia kampeni mgombeaji wa chama cha JAP Philip Charo mpaka harakati za kampeni zifike ukingoni.
Wakiongea siku ya Jumanne katika hafla za kumfanyia kampeni mgombeaji wa chama cha JAP Philip Charo katiko eneo Bunge la Malindi, wabunge hao waliwataka wananchi kupiga kura kwenye upande wa serikali kwa Philip Charo iwapo wanataka kuendelea kupata miradi ya maendeleo kutoka kwa serikali ya JAP.
Hata hivyo, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amewasuta waasi hao na kusema kuwa wanajitafutia umaarufu na kuwahimiza wenyeji wa eneo bunge la Malindi kutoyumbishwa na vuguvugu la chama cha JAP.
Joho alidai kuwa viongozi hao wana nia tu ya kupata kura na hawana maendeleo ya kuwaonyesha wakaazi.
Aliwataka wakaazi kupiga kura kwa wingi kwa Willy Mtengo kwenye uchaguzi ambao unatarajiwa kufanywa tarehe 7 mwezi huu.