Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa kisiasa katika eneo la Pwani wameshinikizwa kuweka tofauti zao za kisiasa kando na kuungana na Tume ya kitaifa ya Ardhi nchini NLC ili kutatua swala la uskwota.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa vijana wa kimijikenda eneo la Pwani Nguma Charo, alisema kwamba iwapo viongozi hao wana azma ya kuwatetea wapwani katika swala la ardhi, basi ni lazima kujitolea kikamilifu na kuungana.

Charo alisema kwamba mwenyekiti wa tume hiyo ya ardhi Dkt Mohamed Swazuri anafaa kuungwa mkono kikamilifu kwani swala la ardhi ni swala la kihistoria hiyo basi akisaidiwa tatizo hilo litapata suluhu la kudumu.

“Viongozi wetu wanafaa kujitokeza waziwazi na kuiunga mkono tume ya kitaifa ya ardhi na kulitatua tatizo hili kwa pamoja, ili kusitisha uskwota hapa Pwani. Bila ya kuungana basi wakazi wa Pwani watazidi kukandamizwa,” alisema Charo.

Wakati huo huo aliwataka wabunge wa Pwani kuwashawishi wabunge wenza kupinga mswada wa ardhi ya jamii uliowasilishwa bungeni.

Alisema kwamba mswada huo huenda ukawakandamiza wananchi na kupendakeza mamlaka ya ardhi kubaki katika tume ya ardhi.

“Tunawaomba wabunge wa Pwani kuwashawishi wabunge wenza kuupinga mswada wa ardhi ya jamii kule bungeni kwa sababu iwapo mswada huo utapishwa, basi wapwani tutakosa haki yetu ambayo tumekuwa tukiipigania tangu jadi,” alisema Charo.

Alisema kuwa swala la mizozo ya ardhi katika eneo la Pwani limekuwa donda sugu kutokana na swala hilo kuwa la kihistoria, licha ya serikali kujitokeza na kuwaahidi wapwani kulitatua swala hilo na kuwapa wapwani hati miliki.