Shughuli za kawaida zilikwama kwa muda kwenye barabara kuu ya Kisii-Nairobi siku ya Jumatatu, baada ya waendeshaji bodaboda kufanya maandamano kulalamikia hali mbaya ya usalama katika eneo hilo.
Kiongozi wa waendeshaji bodaboda hao Wilson Motari alisema kuwa walilazimika kuchukua hatua hiyo ya kuziba barabara kutokana na hali ya kudorora kwa usalama katika eneo hilo.
Alirejelea kisa cha hivi majuzi ambapo waendeshaji bodaboda wawili walishambuliwa siku ya Jumapili na watu wasiojulikana.
"Ni jambo la kukasirisha kujua kuwa hamna mtu anayejihusisha na usalama wetu. Wengi wetu wamepoteza pesa na ata pikipiki zao baada ya kuvamiwa na genge fulani la watu wasio julikana. Wawili wetu walichapwa siku ya Jumapili na kuachwa na majeraha,” alisema Motari.
Motari alidai kuwa walilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya maafisa wa polisi kufeli kuimarisha doria katika eneo hilo, kuhakikisha kuwa wahalifu hao wametiwa mbaroni.
"Tuna watoto na sisi hutegemea sana biashara hii ili kulisha familia zetu. Sisi hulipa ushuru ili kuhakikishiwa usalama na serikali lakini hamna hatua yeyote maafisa wa polisi wamechukua kuhakikisha kuwa wahalifu wanao tuhangaisha wametiwa mbaroni, hata baada yetu kulalamia hali ya usalama eneo hili," alisema Motari.
Hata hivyo, OCS wa Matutu, Benjamin Mutinda, alisema kuwa polisi wameanzisha msako mkali ili kuwanasa washukiwa hao wa uhalifu.
Aliwaonya waendeshaji bodaboda kuasi tabia ya kufanya kazi hadi usiku wa manane.
"Tunafanya juhudi kuhakikisha kuwa tunawanasa washukiwa wa uhalifu wanao wahangaisha waendeshaji bodaboda katika eneo hili. Ni ombi letu kwenu kusitisha shughuli za kufanya biashara hadi usiku wa manane kwa kuwa baadhi ya wahalifu hujifanya kuwa wasafiri na kisha baadaye kuwageukia na kuwashambulia," alisema Mtinda.