Baadhi ya wafanyikazi wa kitambo wa manispaa ya Nyamira wangali kulipwa madeni ya mishahara yao ya takribani shillingi millioni 490.
Wakihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumamosi, wafanyikazi hao waliipa serikali ya kaunti hiyo makataa ya mwezi mmoja kusuluhisha hali hiyo, la sivyo waelekee mahakamani.
"Tulifanyia manispaa ya Nyamira kazi wakati wa mwaka wa uchaguzi 2013 ila hatukulipwa mishahara yetu, na kwa mda sasa tumekuwa tukiiomba serikali ya kaunti kutulipa pesa zetu bila mafanikio, na kwa sasa tunaipa serikali makataa ya mwezi mmoja kutulipa pesa zetu la sivyo tuichukulie hatua za kisheria," alisema mwenyekiti wa wafanyakazi hao Moses Okebiro.
Okebiro aidha aliongeza kwa kusema kuwa mamlaka ya mpito ndiyo iliyohujumu mipango ya wafanyikazi hao kulipwa madeni yao mamlaka ambayo ilikuwa imeahidi kuwa wangelipwa mishahara yao.
"Mamlaka ya mpito ndiyo inayohujumu matakwa yetu ya kulipwa mishahara yetu ilhali ndiyo iliyotuhaidi kuwa ingehakikisha kuwa tumepata haki yetu na sasa tumechoka, na ndio maana tunaitaka serikali ya kaunti kutulipa, la sivyo iwe tayari kukutana nasi mahakamani," aliongezea Okebiro.
Wafanyakazi hao ambao kwa sasa wanafanyakazi chini ya uongozi wa serikali ya kaunti vilevile waliishtumu serikali ya kaunti kwa kutochukua hatua ya kuwapandisha vyeo.
"Ni kama serikali ya kaunti inataka kutuhujumu kwa kukataa kutupandisha vyeo kulingana na na kipengee cha tume ya wafanyikazi wa umma PSC," alihoji Okebiro.