Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa Idara ya Utalii na Biashara katika kaunti ya Kisumu Rose Kisia, amewataka wakaazi wa Kisumu na eneo la Nyanza kwa jumla, kujivunia utamaduni wao na kuupitisha kwa vizazi vijavyo.

Kisia alisema kuwa sekta ya utalii itapiga hatua kubwa katika eneo la Nyanza, iwapo utamaduni utazingatiwa na kudumishwa ipasavyo.

Akizungumza katika uwanja wa Jomo Kenyatta jijini Kisumu siku ya Jumatano, wakati wa sherehe za utamaduni wa jamii ya Waluo, Kisia alisema kuwa ni jukumu lao kama serikali ya kaunti kuendeleza utamaduni katika kaunti ya Kisumu, na eneo la Nyanza kwa jumla.

“Hafla hii ya utamaduni ni mwanzo wa safari ndefu ya kutambua, kukuza na kuhifadhi utamaduni wetu kama watu wa Nyanza,” alisema Kisia.

Ni mara ya kwanza kwa sherehe za utamaduni wa jamii ya Waluo kuandaliwa, huku hafla hiyo ikihudhuriwa na viongozi kadhaa wa eneo la Nyanza.

Kennedy Otieno, mkaazi wa Kisumu, aliyehudhuria sherehe hizo katika uwanja wa Jomo Kenyatta, aliwataka wakaazi wa Nyanza kujitokeza kwa wingi kujifunza mengi kuhusiana na utamaduni wao.

“Hafla hii inafaa kutumiwa kutoa mafunzo kuhusu maadili mema na utamaduni, ili vizazi vijavyo vione sababu ya kuzingatia utamaduni wetu,” alisema Otieno.

Otieno alitoa wito kwa serikali za kaunti za Kisumu, Migori, Siaya na Homabay, kuandaa sherehe hizo kila mwaka, kama njia moja ya kuwaleta pamoja wananchi wa jamii ya Luo.