Wakulima wa majani chai katika eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini wameombwa kuwa watulivu kuhusu ujenzi wa kiwanda kipya cha majani chai katika eneo la Sombogo.
Hii ni baada ya ujenzi wa kiwanda hicho kuchukuwa muda mrefu bila kuanza baada ya mikakati kuimarishwa hapo mbeleni ili kiwanda hicho kujengwa.
Akizungumza na mwandishi huyu mnamo siku ya Jumatano mjini Kisii, mwakilishi wa wadi ya Sensi Onchong’a Nyagaka alisema serikali ya kaunti ya Kisii ilitenga shillingi millioni 30 ili kufadhili ujenzi huo, huku akiomba wakulima wa majani chai na wakazi kuwa watulivu na kuahidi ujenzi huo kuanza hivi karibuni.
Malalamishi yamekuwa yakitolewa na wakulima hao pamoja na wakazi wengine kwa serikali ya kaunti pamoja na halmashauri ya majani chai nchini.
“Naomba wakulima wa majini chai kuwa na subira na kuwa watulivu maana ujenzi wa kiwanda hicho utaanza karibuni,” alisema Nyagaka.
“Serikali ya kaunti ya Kisii itashirikiana na KTDA ili kuhakikisha kuwa ujenzi huo unafadhiliwa maana serikali ya kaunti tayari imetenga millioni 30 kusaidia ujenzi huo,” aliongeza Nyagaka.