Hali ya wasiwasi inaendelea kushuhudiwa miongoni mwa wanafunzi wa shule ya upili ya Nakuru ya wavulana baada ya mojawapo wa bweni ya shule hiyo kuteketea siku ya Jumatano.
Afisa wa elimu katika kaunti ndogo ya Nakuru Eunice Khaemba aliahidi kuwa wanafunzi watapata ushauri wa kutosha.
Khaemba akizungumza na wanahabari chuoni humo siku ya Alhamisi alielezea kuwa wizara ya elimu itafanya uchunguzi wa kina na kuja na ripoti kamili kuhusu kisa hicho.
‘Ni tukio la kusikitika sana ila tunashukuru maulana hakuna mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa katika mkasa huo. Hata hivyo tumeweka mikakati dhabiti kuhakikisha wanafunzi hao wanapewa ushauri wa kutosha kwa wale walioathiriwa.’ Khaemba alielezea wanahabari chuoni humo.
Khaemba pia amewahakikishia wazazi kuwa wanafunzi 42 waliokuwa wakiishi katika bweni hilo watapewa makao mbadala huku shule hiyo ikiendelea kutatua shida hiyo.
Uchunguzi hata hivyo inadokeza kuwa moto huo ulizuka kutokana na hitilafu ya umeme katika bweni hiyo.