Huku sakata ya mamilioni ya fedha za Shirika la huduma ya Vijana kwa taifa( NYS) ukichukua mkondo mpya, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir aliwataka wale wote wanahusishwa na sakata hiyo kujiuzulu.
Akizungumza katika eneo la Ganjoni alipoongoza zoezi la kulisafisha eneo hilo siku ya Jumamosi, Nassir alisema kuwa wizi huo wa mamilioni ya fedha za umma unaashiria wazi jinsi Serikali imesheheni ufisadi.
Nassir alisema kuwa bila ya Wakenya kuwa macho na kufanya mageuzi muhimu ya uongozi wa taifa hili, kashfa za ufisadi zitashamiri.
Mbunge huyo wa Mvita alisema kuwa viongozi wanaohusishwa na sakata hiyo akiwemo kiongozi wa walio wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen wanapaswa kuondoka mara moja mamlakani.
“Wale wote waliohusishwa na sakata ya ufisadi wajiuzulu ili kutoa nafasi ya uchunguzi,”alisema Nassir.