Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kamati ya Bunge kuhusu uchukuzi na miundo msingi nchini imesema itawaita wasimamizi wa Shirika la huduma za feri KFS nchini kueleza bayana kinachaendelea katika kivuko cha feri cha Likoni.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Maina Kamanda, aliyasema hayo baada ya kufanya kikao cha faraga na wasimamizi wakuu wa shiriki hilo ikiwemo Mkurugenzi mkuu Hassan Musa, Mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo James Fondo na wasimamizi wengine wakuu.

Akiongea na wanahabari baada ya vikao hivyo katika afisi za shirika hilo mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Kamanda alisema kwamba lazima wasimamizi wa shirika hilo kufika mbele ya kamati hiyo jijini Nairobi na ripoti za usimamizi duni kuidhinishwa.

Aidha, alisema kwamba japo serikali inahitajita kutoa fedha kwa shirika hilo ili kukarabati feri zinazokumbwa na hitilafu za kimitambo, kuna haja ya ushirikiano mwema baina ya wasimamizi wakuu na wafanyikazi wa shirika hilo ili kuwahudumia wakazi wanaotumia kivuko hicho.

“Tunajua kuwa hapa kunahitaji pesa za kutosha na hilo tutalitekeleza lakini lazima wasimamizi wa shirika hili wafike mbele ya kamati ya mbunge kule Nairobi na kueleza bayana kinachoikumba huduma za kivuko cha feri cha Likoni,” alisema Kamanda.

Wakati uo huo, alimkosoa Katibu katika Wizara ya Uchukuzi na Miundo msingi, John Mosonik, kutokana na matamshi yake ya kumtaka Kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa kukoma kuingilia shughuli za kivuko cha feri huku akisema kwamba afisi zote za umma zinawakilishwa na Kamishna huyo mbele ya serikali kuu.

“Mwanzo Katibu katika Wizara ya Uchukuzi amefanya makosa makubwa sana kwa sababu kaunti kamishna ndiye mshirikishi mkuu wa afisi zote za serikali kuu na ni makosa makubwa kwa Mosonik kusema Marwa asiingilie shughuli za feri,” aliongeza Kamanda.

Kamanda alisema kwamba Kamishna Marwa anafahamu vyema utepetevu unaoendelea katika kivuko hicho pamoja na afisi za shirika hilo, na lazima hatua za dharura zichukuliwa ili kuzuia kutokea kwa majanga katika kivuko hicho.