Washirika wa dhehebu la Toba na utakatifu linaloongozwa na Nabii David Owuor wamefanya mkutano wa dharura Jumamosi kutubu, baada ya kudaiwa mmoja wao jijini Nairobi amekuwa akipanga kumuua Owuor.
Waumini wa dhehebu hilo Nakuru walikusanyika katika madhebau ya Maonyesho ya Kilimo Nakuru chini ya Askofu mkuu Onjoro na kutubu kwa niaba ya muumini huyo anayedaiwa kuzuru nyumbani kwa Nabii Owuor jijini Nairobi akiwa na njama ya kumwangamiza.
Akiongoza ibada hiyo ya toba, Askofu Onjoro alidokeza habari hizo kwa waumini waliokuwa kwa magoti wakitubu.
"Muumini anayedaiwa kuwa na njama ya kumuua Nabii Owuor amekuwa akifuatilia mikutano yote na hata wakati mmoja njama yake ilitibuka uwanjani Afraha baada ya Nabii Owuor kutumia njia tofauti kuondoka uwanja huo," alisema Onjoro.
Wakati huo huo, askofu huyo alikosoa vyombo vya habari namna vinavyoripoti kuhusu mikutano ya Nabii Owuor, huku akirejelea ripoti katika baadhi ya majarida ya humu nchini kwamba Nabii Owuor alitumia sufuria kuomba fedha katika mojawapo wa mikutano.
Onjoro alifafanua kuwa hamna fedha zozote ambazo husanywa, wala hata sadaka katika mikutano ya uponyaji.