Baadhi ya wakaazi wa kijiji cha Riamanoti, Kaunti ya Nyamira, wamemtaka kamishna Josphine Onunga kuingilia kati na kuhakikisha kuwa vijana wanaojiunga na makundi ya uhalifu wanatiwa mbaroni.
Wakihutubu kwenye mkutano wa dharura siku ya Jumatano wakati wazazi wanne wa eneo hilo walipojitokeza kueleza masaibu yao baada ya wanao kutoweka bila ya kufahamika waliko, wazazi hao walimsihi Onunga kuchukua hatua ili kuhakikisha kuwa vijana waliotoweka manyumbani mwao wanasakwa ili wahojiwe kuhusiana na kundi la uhalifu linalo wahangaisha wakazi wa Borabu.
"Uhalifu unaendelea kukithiri katika eneo hili, na ndio maana tunamtaka kamishna Onunga kuchukua hatua ya kuwasaka vijana wetu ambao tunakisia kuwa wamejiunga na makundi ya uhalifu yanayotuhangaisha," alisema mnenaji wa wazazi hao, John Makori.
Wazazi hao aidha walisema kuwa iwapo serikali haitochukua hatua za haraka kurekebisha hali hiyo, huenda vijana wengi wakajiunga na makundi ya uhalifu.
"Tunaiomba serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa vijana waliopotea manyumbani mwao wamepatikana kwa kuwa hilo lisipofanyika, huenda vijana hao wakajiunga na makundi ya kigaidi," aliongezea Makori.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wadi ya Nyansiongo, Jackson Mogusu, aliwapongeza wazazi wa eneo hilo kwa hatua waliyochukua ili kuifahamisha serikali kuhusiana na kutoweka kwa wanao.
Mogusu aliahidi kuwasiliana na kamishna wa kaunti hiyo ili kuhakikisha kuwa vijana hao wamesakwa.
"Ni jambo nzuri kujua kuwa wazazi wamejitokeza kuripoti kuwa wanao wametoweka. Nitazungumza na kamishna wa kaunti ili kuhakikisha kuwa vijana waliotowekwa wanasakwa kwa kuwa tumechoshwa na visa vya uhalifu katika eneo hili," alisema Mogusu.