Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wazazi kaunti ya Nakuru kaskazini ambao wanao hutegemea msaada wa basari kulipa karo wameiomba Serikali ya jimbo la Nakuru kupitia gavana Kinuthia Mbugua iharakishe shughuli za kutoa msaada huo kabla muhula huu wa kwanza kutamatika.

Kulingana na wazazi hao, kuna uwezekano mkubwa wanao wakafukuzwa shuleni hasa mwishoni mwa mwezi huu wa Januari kutokana na kutolipa karo hivyo.

Wakizungumza Jumatano, wazazi hao waliitaka serikali kuchukulia swala hilo kwa udharura.

“Tunamlilia gavana Mbugua na mbunge wetu kuweza kusikia kilio chetu maanake hatuna mahala pengine pa kukimbilia,” Tabitha Njeri alisema.

Aidha katika siku za hivi karibuni mwakilishi wa wadi ya Kabazi Mwangi Waithaka alimtaka gavana Mbugua kuharakisha shughuli za kutolewa kwa fedha hizo baada ya kupokea lalama kutoka kwa wazazi wakipendekeza msaada huo uwe ukitolewa wakati wa likizo ili wanafunzi wasiwe wakitumwa nyumbani wakati masomo yanaendelea.