Mwanasiasa katika eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira Victor Ogeto ameomba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuchunguza madai ya wanasiasa ambao wananunua na kuleta wakaazi kutoka eneo bunge zingine kujisajili kama wapiga kura katika eneo la kitutu Masaba.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya wakaazi ambao ni wa maeneo ambayo yako karibu na bunge hilo na wamejisajili Kitutu Masaba kwa kuwa wana nia ya kuchagua viongozi fulani katika eneo hilo
Akizungumza siku ya Jumapili katika eneo bunge hilo, Ogeto aliwalahumu wanasiasa hao ambao huwaleta wakaazi hao ili kupigiwa kura katika uchaguzi wa mwaka ujao.
Ogeto ametilia shaka jinsi usajili wa wapiga kura unavyoendeshwa, akidai kuwa hauna uwazi na haki na ametaka uchunguzi ufanywe ili hatua zichukuliwe dhidi ya wanaokiuka sheria.
Kulingana na Ogeto ni haki kwa mkaazi kujisajili popote lakini jinsi suala hilo limechukuliwa si kwa njia ya kupendeza ila ni mzaha.
“Naomba tume ya IEBC ichunguze kwa nini swala hili la uhamisho kwa wanaojisajili kama wapiga kura limeongezeka,” alisema Ogeto.
“Jinsi usajili huu unaendeshwa hauna haki maana hapa Kitutu Mabasa wengi ambao wamejisajili si wa eneo bunge hili tunaomba uwazi na haki kutendeka,” aliongeza Ogeto.