Seneta wa kaunti ya Nyamira Okong'o Mong'are amejitokeza kusema kuwa ili tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC iafikie idadi ya wapiga kura inayonuia kusajili sharti ibuni mbinu yakutembelea watu vijijini.
Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya jumamosi Mong'are alisema kuwa kufuatia idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kwenye vituo vya kusajili watu kuwa wapiga kura shartitume hiyo ianzishe mpango wakutembelea watu kwenye hafla mbalimbali ili kufanikisha zoezi hilo.
"Kwa wiki tatu sasa na ni idadi ndogo tu ya watu ambao wamekuwa wakijitokeza kwenye maeneo ya usajili wa wapiga kura," alisema Mong'are.
"ndio maana naona ni muhimu kwa tume ya IEBC ianzishe mikakati yakutembelea sehemu za hafla za mazishi, arusi na hata mikutano ya umma ili angalau kuwafikia watu wanaonuia kuwasajili," aliongeza Mong'are.
Mong'are aidha aliwapa changamoto wakaazi wa kaunti ya Nyamira kuhakikisha kuwa wanasajiliwa ili kuwachagua viongozi wanaowataka kwenye uchaguzi mkuu ujao.
"Ili kuwachagua viongozi mnaowataka kwenye uchaguzi mkuu ujao sharti muwe na silaha ambayo ni kadi yakupiga kura na hilo halitawezekana iwapo hamtajitokeza kujisajili kama wapiga kura," alisema Mong'are.