Mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi Samuel Arama ametoa wito kwa idara ya usalama katika kaunti ya Nakuru kuhakikisha kwamba hakuna anayeleta vurugu katika vituo vya usajili wa wapiga kura, hasa zoezi hilo linapoelekea kukamilika.
Katika kikao na wanahabari siku ya Jumanne, Arama alisema kuwa idara ya polisi inafaa kuhakikisha kwamba shughuli hiyo iliyoanza kwa njia ya amani inakamilika kwa utulivu pasina vurugu zozote.
"Shughuli hii inapoelekea tamati huenda kuna wale ambao watajitokeza kujaribu kuleta vurumai na sintofahamu katika vituo vya usajili wa wapiga kura. Tunawaomba maafisa wetu wa polisi kuhakikisha kuna usalama wa kutosha,” alisema Arama.
Matamshi yake yanajiri wakati ambapo zoezi hilo linatarajiwa kukamilika tarehe Machi 15, kwa mujibu wa taarifa ya IEBC kwa vyombo vya habari.
Wakati huo huo, Arama ametoa wito kwa vijana na akina mama katika eneo bunge lake kuhakikisha kwamba wanajiandikisha kama wapiga kura, kabla ya zoezi hilo kukamilika ili wapate fursa ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao.
Isitoshe, amewahakikishia wakaazi wa eneo bunge hilo kwamba atazidi kujitolea kuwahudumia huku akiwa na imani ya kurejea bungeni katika uchaguzi mkuu ujao.