Azma ya seneta mteule wa Kaunti ya Mombasa Emma Mbura kutaka kuwania wadhifa wa uwakilishi wa wanawake katika kaunti jirani ya Kilifi unaonekana kukumbana na changamoto.
Hii ni baada ya baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo ya Kilifi kuonekana kutofautiana na mpango huo wa seneta huyo.
Akiongea na wanahabari siku ya Jumatatu, Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi Keneth Kamto alisema kuwa itakuwa bora iwapo kiongozi huyo ataendelea kuwakilisha Kaunti ya Mombasa.
Kwa upande wake, Mbura, ambaye ni mzaliwa wa kaunti hiyo ya Kilifi aliendelea kukashifu viongozi wa kaunti hiyo, huku akisema kuwa hawana maono ya maendeleo.
“Mimi nimeamua kurudi nyumbani mahali nilikozaliwa kwa sababu nimeona hakuna mtu anayeleta mabadiliko eneo hilo,” alisema Mbura.
Seneta huyo pia aliongeza kuwa anashangazwa na jinsi eneo la Rabai linavyoendelea kuzoroteka kielimu wakati historia inaonyesha kuwa shule ya kwanza eneo la Pwani ilianzishwa eneo hilo.
“Ikiwa sote tunajua kuwa ustaarabu ulianzia Rabai na sisi tunaangalia tu eneo hilo likibaki, nyuma basi itakuwa aibu kubwa sana kama viongozi,” aliongeza Mbura.
Azma ya Mbura kuwania kiti hicho ilianza miezi michache iliyopita baada ya kuonekana kulaumu viongozi wa kaunti hiyo akidai kuwa wanalemaa katika kuleta maendeleo katika kaunti hiyo.