Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Uhuru Kenyatta amewahidi wakazi wa eneo la Pwani kuwa barabra ambayo imekuwa ikileta gumzo kwa muda sasa ya Garseni-Garrissa itaanza hivi karibuni ili kuwafaa wakazi wa maeneo hayo.

Akiyahutubia zaidi ya makundi 50 ya vijana kutoka kaunti mbali mbali za eneo la Pwani rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa atafahamisha wizara husika ya barabara ifanye kila linalowezekana ili kuona kuwa barabara hiyo imeanza msingi wake haraka na kuongeza kuwa hali zote za barabara katika maeneo ya Pwani zitashughulikiwa.

Rais pia alidokeza kuwa barabara ambazo zinaendelea chini ya mradi wa serikali za Witu hadi Kwale na baadhi ya barabara ambazo bado zinahitaji kukarabatiwa zitaangaliwa chini ya miradi ya serikali ya kuboresha na kuimarisha miundomsingi katika kila maeneo si tu Pwani.

“Barabara zote ambazo zinajengwa zitaharakishwa, na barabara ya Garseni kuenda Garrissa na ile ya Witu ambayo inaendelea wizara husika nimeamuru iharakishe miradi hiyo ili kuwafaidi wakazi wa maeneo hayo husika,” alisema kiongozi wa nchi.

Rais Uhuru amekuwa kwenye eneo la Pwani tangu mwanzo wa wiki hii na anatarajiwa kuzuru Kaunti ya Lamu kuanzia Alhamisi ili kujadiliana na vingozi wa Kaunti hiyo kuhusiana na masuala ya uongozi na maendeleo.