Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa kina mama kutoka kaunti ya Nyamira Alice Chae amejitokeza kutetea kamati ya wanachama watano aliowateua kwenye bodi ya kuangalia matumizi ya shillingi millioni 28, pesa zilizopokezwa kaunti zote ili kufanya miradi muhimu ya maendeleo.

Akihutubia wakazi wa Magombo siku ya Jumanne, Chae alisema kuwa wanachama hao waliteuliwa kwa misingi ya taaluma zao kwa kuwa watasaidia pakubwa katika kuanzisha miradi mhimu itakayowasaidia vijana na kina mama wa kaunti hiyo kujistawisha.

“Sidhani kuwa nilizingatia ukoo wakati nilipoteua wanakamati wa bodi kwa maana nililozingatia wakati wa uteuzi ni hakikisho la kufanya kazi na watu ambao wamekuwa wakifanya kazi na makundi ya kina mama na nina hakika kuwa watanisaidia kuanzisha miradi muhimu itakayo wasaidia kina mama na vijana katika kaunti hii,” alisema Chae.

Chae aidha alisema kuwa maeneo kaunti zote ndogo za kaunti ya Nyamira ziliwakilishwa kwenye kamati hiyo, huku akiyasuta madai ya kuwa na mapendeleo kwenye uteuzi wake.

“Kaunti zote ndogo ziliwakilishwa kwenye kamati, na suala langu kuwajua baadhi ya wanakamati halimaanishi kwamba nina mapendeleo na wale wanaonipinga wanafaa kujiunga nami ili tushirikiane kustawisha maisha ya wakazi,” aliongezea Chae.