Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu uchukuzi na miundomsingi nchini Maina Kamanda ameitaka tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini kuzuru afisi za shirika la huduma za feri nchini na kuchunguza shughuli za shirika hilo.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Kamanda alisema kwamba usimamizi duni unayoshuhudiwa katika kivuko cha feri huenda ukawa unachangiwa na kukithiri kwa kashfa za ufisadi kwani hatua hiyo wataeleza bayana chanzo cha kushuhudiwa msongomano wa magari na abiria katika kivuko hicho.

Kamanda amesema kwamba utoaji wa zabuni za ununuzi wa vifaa vya kukarabati feri hizo huenda zikawa zinatolewa kwa njia ya ufisadi, huku akiongeza kwamba wizara ya uchukuzi na miundo msingi imekosa kuwajibikia majukumu yake vyema na kuchangia mgogoro huo.

"Tume ya EACC lazima ije hapa na kuchunguzi shughuli za kikazi za shirika hili la feri pamoja na utoaji wa zabuni na kandarasi kwa baadhi ya makampuni kwani huenda ikawa chanzo cha kushuhudiwa utata huu, na bila ya swala hili kuchukuliwa kwa makini, basi wananchi wetu watazidi kuumia sana," alisema Kamanda.

Kamanda aliongezea kuwa amebaini kutokuwepo na ushirikiano mwema baina ya viongizi wa shirika hilo la huduma za feri na wafanyikazi wanaohudumu katika feri hizo, na akasema kwamba malumbano yanayoendelea chini kwa chini yanafaa kusitishwa na wafanyikazi kushirikiana vyema.

Haya yamejiri baada ya kushuhudiwa mkanyagano katika kivuko cha feri cha Likoni siku chache zilizopita na kusababisha majeraha ya watu 15 baada ya feri ya MV Kwale kukumbwa na hitilafu za kimitambo na kuwepo kwa feri moja ya kuhudumu.