Familia moja katika shule moja ya kibinafsi iliyoko Naivasha imetishia kufungulia shule moja katika eneo hilo mashtaka kwa kile wamedai kuwa kuficha jaribio la unajisi kwa binti wao ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu.
Akieleza matukio yalivyojiri msichana huyo mwenye umri wa miaka 17 amesema kuwa mtu asiyetambulika aliingia katika bweni lao akiwa amejihami na kuwatishia kuwaua iwapo wangepiga kelele.
Tukio hilo linadaiwa kufanyika tarehe 14 mwezi Januari mwaka huu.
Msichana huyo ameeleza vyombo vya habari kuwa mshukiwa alimshika mkono na kujaribu kumtoa nguo huku akimtishia iwapo atapiga kamsa lakini vuta nikuvute kati yao iliwaamsha wenzake waliomwokoa.
Ametaja kuripoti kisa hicho kwa mwalimu mkuu lakini hakuna hatua iliyochukuliwa mbali na kutishiwa kufukuzwa shuleni kwa misingi kuwa madai yake yalikuwa ndoto.
Akiongea na wanahabari, mwalimu mkuu wa shule ya wasichana ya St Francis Xaviers Ruth Kahiga amekiri kuwa kisa hicho kilifanyika.
“Tuliweza kuripoti kisa hicho kwa maafisa wa polisi na kwa kiwango fulani madai ya msichana huyo yalikuwa na utani,” alisema Bi Kahiga, akihojiwa na wanahabari.
Ametaja swala la siasa kuingizwa katika tukio hilo japo amedinda kufafanua kwa vyombo vya habari kivipi siasa ziliingizwa katika swala la unajisi.
Kulingana na babake msichana huyo ambaye alitaka jina lake kubanwa, ni kuwa hatua ya mwalimu mkuu kutoa taswira mbaya ya mwanaye sio la busara ilhali anatambua yaliyojiri.
“Kisa hicho kumemwathiri mwanangu na ningependa wizara ya elimu nchini kuchunguza kisa hiki kwa lengo la kuhakikisha usalama kwa wasichana wetu shuleni,” alisema babake msichana huyo.