Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Nakuru, Kinuthia Mbugua, amewapongeza wakazi wa Nakuru kwa kushirikiana na serikali ya kaunti katika kuhakikisha kuna oungozi mwema.

Akizungumza kwenye makao makuu ya Kaunti ya Nakuru siku ya Jumanne, Gavana Mbugua aliwashukuru wakazi wa Nakuru kwa kuhakikisha serikali yake inapata wakati rahisi wa kuwahudumia.

Wakati huo huo, aliwahimiza kufanya uamuzi wa busara wakati wa kupiga kura ya uchaguzi akiongeza kuwa wananchi watatathmini utenda kazi wa serikali ya kaunti ya Nakuru wakati wa kupiga kura.

“Mlituajiri kazi na mmeturuhusu tufanye kazi hiyo. Hampigi Kelele ovyo ovyo na ile Kelele ambayo mnapiga ni ya kuturekebisha na kusema tuangalie pande mbalimbali. Mtafanya utathmini na kutoa ripoti yenu baada ya miaka mitano na hapo ndipo ninapowaheshimu sana kwa sababu hatuwezi kusema tulitaka kufanya kazi kisha mkatukataza,” alisema Mbugua.

Mbugua alisema kwamba maandamano yanaruhusiwa huku akitoa wito kwa wakazi kutojihusisha katika maandamano yasiyofaa na badala yake kuwataka wawajibike ipasavyo.

“Hatusemi kufanya maandamano ni makosa lakini kuna wakati wa maandamano. Maandamano mengine yanajulikana na watu wawili au watatu ambao wamelipwa na wanaowahamasisha watu na kisha pesa hizo wanaweka mfukoni,” alisema Mbugua.

Haya yanajiri baada ya kundi moja la kijamii kuiitisha maandamano kumshinikiza Gavana Mbugua kutojitokeza kuelezea kuhusu madai ya utumizi mbaya wa fedha, kwa mujibu wa ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu ya mwaka wa kifedha wa 2013/2014.