Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamume mmoja mwenye umri wa makamo ameripotiwa kuuwawa kwa kudungwa kisu na mwenzake, kwa madai ya kugombea mwanamke katika kijiji cha Mwambao, eneo bunge la Lungalunga.

Marehemu, Mwinyihijjah Shee, anaripotiwa kudungwa kisu na Hamadi Kisupi, kwa madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wake wa zamani.

Akidhibitisha kisa hicho siku ya Jumatatu, mkuu wa kituo cha polisi cha eneo la Lungalunga,  Abdullah Tato, alisema kuwa inaripotiwa marehemu alivamiwa na kushambuliwa na kijana huyo mwendo wa saa saba usiku katika makaazi yake.

Tato alisema kuwa marehemu alikuwa amedungwa kisu mara tatu katika sehemu ya shingo, tumbo na kifua.

Taarifa iliyoandikishwa na mwanamke anayedaiwa kuwa chanzo cha mgogoro huo ulieleza kwamba aliachana na mshukiwa  na kisha kuanza uhusiano na marehemu.

Mwanamke huyo alidai kuwa hiyo ndiyo sababu mshukiwa amekuwa akimtishia kumuua jamaa huyo iwapo asingeachana na mchumba wake wa zamani.

Kwa sasa mshukiwa huyo ameenda mafichoni huku polisi wakianzisha msako.