Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya wanawake duniani, akina mama na vijana pamoja na jamii kwa jumla wamehimizwa kujitokeza na kushirikiana kufanikisha siku hii.
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake Pwani (Coast Women in Development) Betty Sharon, amesema kuwa siku hii ni muhimu sana kwa wanawake na kuna haja ya jamii kujitokeza ili kujulishwa mengi kuhusu haki za wanawake na kuwasaidia katika kupigania haki zao nchini.
Akizungumza na mwanahabari huyu mjini Mombasa siku ya Jumanne kwa mahojiano kupitia njia ya simu, Sharon alisema kuwa tayari maandalizi ya maadhimisho hayo yamepangwa vyema na shughuli ya kuihamsisha jamii itatekelezwa.
Aliwahimza wakaazi kuungana na wanawake katika kutetea haki zao, kupinga dhulma za kijinsia na unyanyasaji, pamoja na kutetea usawa wa jinsia nchini.
Alisema kuwa hatua hiyo itawapa wanawake fursa ya kujitosa kwenye ulingo wa uongozi na maswala mengi muhimu ya kumfaidi mwanamke.
“Tunawaomba wanawake, vijana na jamii kwa jumla kujitokeza kwa wingi kuadhimisha siku hii ya wanawake ulimwengine ili kufahamishwa mengi yanayomhusu mwanamke kama vile kutetea haki zake pamoja na kupinga dhulma nyingi mwanamke anazopitia,” alisema Sharon.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Tononoka mjini Mombasa huku wageni watabaka mbalimbali wakitarajiwa kujimuaka na wanawake kuadhimisha siku hii muhimu kwa wanawake ulimwenguni.