Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kilifi Bi Aisha Jumwa amewajibu wale waliokuwa wakiuliza maswali tata kuhusu uzinduzi wa barabara ya Fidel Odinga, uliofanywa na kiongozi wa Cord Raila Odinga siku ya Jumatano mjini Mombasa.
Mwakilishi huyo ambaye pia ni mwanachama wa Cord alisema kuwa anaunga mkono uzinduzi huo, akiongeza kuwa ni njia ya kumuenzi kiongozi wa chama, na mwanawe ambaye alikuwa mkakamavu zaidi.
Kuhusu wale waliokuwa wakipinga uzinduzi huo wakisema kuwa badala yake ingepewa jina la Mekatilili wa Menza, Bi Jumwa alisema kuwa kuna barabara nyingi katika mji wa Mombasa, zilizopewa majini yasiyowiana kabisa na eneo la Pwani, na kusema kuwa barabara hizo zinafaa kubadilishwa majina.
Jumwa alitaja barabara ya Jomo Kenyatta katikati mwa jiji kama mfano na kusema kuwa barabar hiyo inafaa kubadilishwa jina na kuitwa Mekatilili, miongoni mwa barabara zingine.
“Mimi nasema ikiwa ni swala la kubadilisha barabara na kuzipa majina mapya, basi tuanze na hii ya Kenyatta Avenue, tuiite Mekatilili, pamoja na barabara zingine ili kuwaenzi Wapwani wenzetu,” alisema Bi Jumwa.
Hata hivyo, matamshi yake hayakupokelewa vyema na baadhi ya wakaazi waliozungumza na mwandishi huyu.
Baadhi yao walitaja matamshi hayo kama yaliyokosa msingi.
“Barabara kama ya Kenyatta inamkumbuka mwanzilishi wa taifa hili hayati mzee Jomo Kenyatta, na hakuna vile inaweza kubadilishwa jina. Afadhali angetaja barabara nyingine na wala sio hiyo,” alisema mfanyibiashara mmoja katika soko la Kongowea.