Share news tips with us here at Hivisasa

Kamati ya bunge la Kaunti ya Uasin Gishu kuhusu biashara imetaka maoni ya wachuuzi kuhusisihwa katika mswada wa uchuuzi mjini humo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Peter Chomba alisema ufanisi wa mswada huo utategemea maoni ya wachuuzi ambao ndio wanaolengwa pakubwa na mswada huo.

Bw Chomba alisema mswada huo wapaswa kuweka mazingira bora kwa wachuuzi badala ya kuwadhulumu.

Akihutubu mjini Eldoret, Bw Chomba alisema wachuuzi huchangia kwa kiwango kikubwa katika mapato ya kaunti hiyo hivyo basi wanapaswa kuheshimiwa kama wanabiashara wengine.

“Hii tabia ya kudhulumu wachuuzi yapaswa kukomeshwa. Wachuuzi huchangia pakubwa katika ushuru wa kaunti hii. Wachuuzi hulipa ushuru wa zaidi ya Sh30,000 ambazo ni pesa nyingi hata kuliko baadhi ya wafanyibiashara ambao hulipia Sh20, 000 kwa mwaka”

Chomba alitaka utawala wa kaunti hiyo kuondoa ukabila katika maswala ya wachuuzi haswa wanapoendeleza msako dhidi ya wachuuzi.

Licha ya tetesi za Chomba ambaye ni mwakilishi wa wadi ya Huruma, waziri wa biashara katika kaunti hiyo Bw Philip Melly alisema sheria hiyo itasaidia kukabiliana na utovu wa nidhamu miongoni mwa wachuuzi mbali na kupunguza msongamano wa wachuuzi katikati mwa mji.

“Hii ni sheria nzuri iwapo itatekelezwa. Changamoto ya wachuuzi katika mji wa Eldoret itakabiliwa vilivyo, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na wahalifu ambao hutumia uchuuzi kuendeleza uhalifu hapa mjini,” alisema Melly.