Wakaazi katika eneo bunge la Bahati wamemtaka kamishna wa Kaunti ya Nakuru Joshua Nkanatha kuwachukulia hatua wafanyikazi wa serikali katika afisi za usajili wanaohusika na ufisadi.
Wakizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, wakaazi hao, wengi wao wakiwa wachimba migodi katika eneo la Bahati, walidai kuwa baadhi ya wafanyikazi katika afisi hizo huitisha rushwa kutoka kwa wananchi ili kuwahudumia hasa wanapojiandikisha kupata vitambulisho vya kitaifa.
“Baadhi ya wafanyikazi katika afisi za usajili katika eneo laBahati wamekuwa wakiwadhulumu wananchi wanaotafuta huduma katika afisi hizo. Watoto wetu pia wamekumbwa na wakati mgumu kupata vitambulisho vya kitaifa ili wajisajili kama wapiga kura,” alisema Francis Kimani, mmoja wa wachimba migodi hao.
Kimani alisema kuwa maafisa hao huomba shilingi mia tatu hadi mia saba ili kutoa huduma kwa wananchi.
Wakaazi hao sasa wamemtaka Nkanatha kuagazia suala hilo na kuwachukulia maafisa hao hatua za kisheria.
“Tunamwomba Nkanatha kufanya uchunguzi haraka ili kuwaadhibu wafanyakazi wanaonyanyasa wakaazi. Huu ni wakati ambao kila mtu anahitaji kujisajili kuchukua kura ili tupate kuchagua viongozi wema,” alisema Kimani.