Wakaazi wa Kaunti ya Kisii wameshauriwa kuwa waangalifu msimu huu wa likizo.
Akizungumza mjini Kisii siku ya Jumanne, kamishna wa kaunti ya Kisii Chege Mwangi, aliomba wakaazi kuwa waangalifu kila wakati msimu huu wa sherehe za krismasi.
Mwangi aliomba wakaazi kushirikiana na maafisa wa polisi kudumisha usalama katika kaunti hiyo.
“Naomba kila mkaazi awe mwangalifu wakati huu wa sherehe za krismasi na mwaka mpya. Mambo ya usalama huanza na mwananchi binasfi kwa hivyo naomba kila mkazi awe macho na kushirikiana na polisi kuhakikisha hali ya usalama iko shwari katika kaunti yetu,” alisema Mwangi.
Wakati huo huo, Mwangi aliomba waendeshaji bodaboda kuwa na nidhamu wanapoendelea na shughuli zao za uchukuzi.
Aidha, aliwataka wahudumu hao wa bodaboda kuwa makini wanapowasafirisha wateja wao na kuwaonya dhidi ya kuendesha pikipiki kwa kasi.
Mwangi alisema kuwa usafiri mzuri ulio na manufaa ni wa mwendo wa upole wala sio wa mwendo wa kasi.
“Nawaomba waendeshaji pikipiki kuwa na nidhamu barabarani mnapowasafirisha wateja wenu. Madereva wa magari pia nawaomba mfuate mtindo huo huo,” alisema Mwangi.