Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kaunti ya Uasin Gishu itatumia kima cha shilingi milioni 26 kujenga kituo cha kisasa cha wazima moto.

Kituo hicho kitajengwa katika mtaa wa Maili Nne kwenye barabara kuu ya Eldoret-Uganda kama njia moja ya kuhakikisha kuwa maeneo ambayo mara kwa mara hukumbwa na mikasa ya moto yanafikiwa kwa urahisi wakati wa dharura.

Afisa mkuu anayehusika na maswala ya ujenzi wa miundo msingi katika kaunti ya Uasin Gishu Bw Nelson Martim alisema tayari mipango ya kuanza ujenzi huo imekamilika.

“Tuna imani kwamba ujenzi wa kituo hiki utakuwa afueni kwa wananchi katika mji wa Eldoret na maeneo ya karibu. Ujenzi huu unatarajiwa kuanza wakati wowote mwaka huu,” alisema Martim.

Hata hivyo, afisa huyo aliwataka wawekezaji katika sekta ya nyumba katika mitaa ya mabanda kuhakikisha kuwa wanafuata utaratibu uliowekwa ili kutoa nafasi kwa maafisa wa kukabiliana na mikasa ya moto kufika katika maeneo ya mikasa mitaani humo bila kizingiti.

Wakati huo huo, chama cha kutetea maslahi ya wapangaji nyumba mjini Elodret kimewataka wamiliki wa nyumba ambao hawazingatii usafi kuimarisha usafi katika nyumba zao.

Katibu mkuu wa chama hicho Bw Benard Nandwa alisema kuna baadhi ya wamiliki nyumba ambao hawana vyoo katika ploti zao.

Nandwa alisema msimu huu wa mvua kuna hatari ya kutokea kwa mkurupuko wa ugonjwa katika mitaa ambako hamna vyoo.