Kaunti ya Nakuru imeanza kufaidika na shilingi milioni 471, zilizotolewa na benki ya dunia, kuboresha mfumo wa usafiri katika miji ya Nakuru, Naivasha na viunga vyake.
Fedha hizo zitatumika kujenga maeneo ya wapita njia katika miji hiyo, pamoja na maeneo yanayofaa kutumiwa na waendeshaji pikipiki na wale wa bodaboda za baiskeli.
Mradi huo ulioanza mwaka jana unazidi kupokelewa vyema na wakaazi wengi wa Nakuru, haswaa madereva wa magari.
Hata hivyo, madereva waliozungumza na mwandishi huyu siku Jumamosi waliitaka serikali ya Kaunti ya Nakuru kupitia kwa Gavana Kinuthia Mbugua kuwaelimisha wakaazi na haswaa waendeshaji wa bodaboda, kuhusiana na umuhimu wa kutumia barabara hizo ambazo wanasema zinasaidia kupunguza msongamano na ajali za barabarani.
Afisa wa Kaunti ya Nakuru anayehusika na maswala ya mipango na miundo msingi Victor Ndereva alisema kuwa zaidi ya ajira 150 zimetokana na mradi huo, huku ajira 30 zikitengewa wanawake.
Isitoshe, alidhibitisha kuwa asilimia 70 ya mradi huo tayari imekamilika akisema kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mnamo mwezi Aprili mwaka huu.
Kwa muujibu wake, mradi huo utasaidia kupunguza misongamano haswaa katika barabara za Oginga Odinga, Moi, na Kanu, zilizoko Nakuru.