Share news tips with us here at Hivisasa

Kijana aliyekuwa anakabiliwa na madai ya kuwa na uhusiano na kundi la al-Shabaab aliondolewa mashtaka hayo na kufunguliwa mashtaka zaidi ya matano ya wizi siku ya Jumatatu.

Luqman Mwashee, alitiwa mbaroni wiki iliyopita na kuzuiliwa rumande kwa siku kumi, kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi, na pia kuhusika pakubwa katika mauwaji ya kigaidi yanayofanyika jijini Mombasa.

Juma lililopita, afisa wa upelelezi Jared Oroko aliambia mahakama kuwa Mwashee na wenzake walikamatwa kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na kundi la al-Shabab, dawa za kulevya na pia kumdunga kisu askari mmoja wakati walipokuwa wakitiwa mbaroni.

Baada ya uchunguzi kukamilika, imebainika kuwa Mwashee anadaiwa kujihami kwa kisu na kuhusika katika wizi wa maelfu ya pesa jijini Mombasa.

Mwashee na wengine ambao hawakuwa mahakamani wanadaiwa kujihami kwa kisu na kumuibia Abdul Musa, simu ya thamani ya Sh11,500 na Sh450 pesa taslimu mnamo Agosti 30, 2015 katika eneo la Majengo.

Mshtakiwa huyo aliyakanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu Susan Shitub na kutozwa dhamana ya Sh500,000.

Kesi yake itasikilizwa Novemba 25, 2015.