Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Idara ya afya na usafi wa umma katika kaunti ya Nakuru Jumatano ilitoa ilani ya siku 21 kwa usimamizi wa kituo cha kupima uzani wa magari cha Gilgil ili kuweka vyoo vya umma la sivyo kifungwe.

Haya yamejiri huku ikiibuka kuwa kituo hicho  ambacho huwahudumia maelfu ya wakenya hakikuwa na choo hata kimoja, huku wanaofika hapo wakijisaidia kwenye msitu ulio karibu.

Haya ni kwa mujibu wa mkuu msimamizi wa maswala ya afya katika kaunti hiyo Samuel King’ori.

“Hali ya sasa katika eneo hilo haipo sawa na huenda ikawa na janga la kiafya kwa watumizi na choo kilichoko eneo hilo ni cha wasimamizi pekee, kwa hivyo abiria na wateja wanaofika eneo hilo hawana mahala pa kujisaidia,” alisema King’ori.

Kwa mujibu wa afisa huyo, idara hiyo ilikuwa imeiandikia usiamizi huo mara kadhaa, lakini hakuna hatua zilizokuwa zimechukuliwa ndiposa ikatoa ilani hiyo.

Mkuu huyo amehoji kuwa kutokana na mvua inayoendelea kunyesha, kinyesi cha binadamu kutoka msitu huo kilikuwa kikioshwa hadi mto Gilgil, na ambao huelekea kwenye ziwa la Naivasha.