Kituo cha polisi kilichozinduliwa mwezi huu katika ufuo mwa Bahari Hindi kwenye eneo la umma maarufu kama Pirates kitaendelea kudumisha usalama katika eneo hilo hadi mwisho wa mwezi huu wenye heka heka nyingi za madhimisho ya siku kuu ya Krismasi na sherehe za mwaka mpya.
Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa, ambaye aliongea siku ya Jumatatu kwenye ziara rasmi katika kituo hicho alisema kuwa usalama utaimarishwa kila kona ya fuo za bahari na kwenye maeneo yote ya kaunti ili kuhakikisha kuwa wakazi pamoja na wageni ambao wanaingia kwenye maeneo ya Pwani kutoka sehemu zote wana usalama wa kutosha.
Kamishna huyo alisema kuwa bado idara mbali mbali za usalama, hasa idara ya polisi, itaendelea na juhudi za kuwatafuta wahalifu kwenye mitaa mbali ambapo wanaaminika kujificha na kuwafungulia mashtaka dhidi ya kujihusisha na vitendo vilivyoharamishwa.
Aidha Marwa alitoa onyo kali kwa makundi ambayo yamekuwa yakiwahangaisha wakazi katika jiji la Mombasa kuwa serakali haitachoka kuwasaka vijana ambao wanavuruga amani.
Alitaja makundi kama vile 'Wakali Kwanza' na 'Wakali Wao' kuwa tishio kubwa kwa usalama wa wakazi wa mitaa ya Likoni. Kisauni pamoja na mtaa wa Majengo, na kuwataka wakazi kushirikiana na idara za usalama ili kuona kuwa visa vya uhalifu vinatokomezwa miongoni mwa jamii.