Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Halmashauri ya Bandari nchini KPA, imesema kuwa tayari imetenga kima cha shilingi milioni 100 kukarabati jumba la kuwakaribisha watalii katika eneo la kwanza la kuegesha meli katika Bandari ya Mombasa.

Akizungumza na wanahabari katika bandari hiyo siku ya Jumatatu, afisa mkuu wa mawasiliano katika Halmashauri ya Bandari ya Mombasa Hajj Maseno, alisema kuwa hatua hiyo imetokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaozuru mjini Mombasa kupitia Bandari ya Mombasa.

Hajj alisema kuwa usimamizi wa Bandari ya Mombasa ulifikia uamuzi huo ili kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inaimarika.

Alisema kuwa mikakati maalum imeandaliwa na ifikapo mwezi wa pili, shughuli hiyo itaanza rasmi.

"Wasimamizi wakuu wa Bandari ya Mombasa wamefanya majadiliano na kuafikiana kuhusu uboreshaji wa sekta ya utalii nchini. Tumetenga shilingi milioni 100 kukarabati jumba la kukaribisha watalii bandarini Mombasa. Shughuli hiyo inastahili kuanza mwezi wa pili ili sekta ya utalii iweze kuimarika zaidi,” alisema Hajj.

Hajj alisema kuwa juhudi hizo zitahakikisha kuwa kuna ushirikiano mwema baina ya KPA, Wizara ya Utalii, Bodi ya Utalii nchini na wadau ili kuboresha zaidi sekta ya uatlii na kuinua uchumi wa nchi.