Kundi lingine la wakimbizi wa ndani kwa ndani limeshtumu maandamano ya maajuzi ya waliodai wao ni wakimbizi kutoka eneo la Nyandarua waliofanya maandamano kuelekea ikulu wakidai kupewa makao mara moja.
Wafuasi hao wa kundi la Peace and Reconciliation la KePRa wamewataka polisi kuwachunguza wakimbizi hao wanaodaiwa kujifanya kwa lengo la kuchukua mahala pa wakimbizi halali ambao hawajapewa makao.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao Stephen Mbugua Muthama wakati wa kikao na wanahabari mjini Nakuru siku ya Jumamosi, viongozi hao wamejitenga na kundi hilo la Nyandarua huku wakiunga serikali mkono kwa mipango yake ya kutaka kuwapa makao kuanzia mwezi wa Februari pindi tu kesi ya naibu wa Rais William Ruto itakapo tamatika.
“Lengo la kundi hilo sio sahihi kwa kuwa wamebaini kuwa Ruto anayehusika na kutupa makao yuko mahakamani nchini Uholanzi na sasa wamepata fursa ya kutaka kulaghai serikali,” alisema Muthama.
Kwa sasa wameitaka serikali kuchunguza wanaoshinikiza suala hilo walilotaja kuwa linaathiri amani ambayo tayari imeundwa katika eneo la bonde la ufa.
Hili ni kundi la pili kujitenga na maandamano hayo kwani mapema wiki hii kundi la Kidipo lilijitenga pia na kundi hilo.