Pendekezo la waziri wa masuala ya elimu nchini Fred Matiang'i kutaka wahubiri wanaotumwa kuhudumu katika shule mbalimbali za umma kuchujwa kabla yao kuripoti katika maeneo yao ya kazi imepata uungwaji mkono kutoka kwa vyama vya walimu nchini KNUT tawi la Masaba.
Kulingana na naibu katibu wa chama cha KNUT tawi la Masaba James Oteki, aliyekuwa akihutubu kule Rigoma wakati wa hafla ya maandalizi ya uchaguzi wa viongozi wa walimu mashinani siku ya Alhamisi ni kuwa yafaa walimu wakuu wa shule mbalimbali wafuate mkondo huo.
"Kuna baadhi ya wahubiri wanaofanya kazi kwa muda wa kudumu katika shule zetu na yafaa wawe watu wanaozingatia maadili mema, na kwa sababu hiyo wafaa wachujwe ili kuhakikisha kuwa wana maadili mazuri," alisema Oteki.
Oteki aidha aliwaomba walimu wakuu wa shule kuanzisha mpango wa kuajiri upya wahubiri hao kama njia mojawapo ya kuimarisha uaminifu miongoni mwa wazazi na wanafunzi.
"Kwa muda tumekuwa tukisikia visa visivyo vizuri na vinavyowahusisha wahubiri, na ndio maana nawapa changamoto walimu wakuu wa shule kuajiri upya wahubiri hao ikiwa tunataka kuinua uaminifu miongoni mwa wanafunzi," aliongezea Oteki.
Kwa upande wake naibu mwekahazina wa chama cha KNUT tawi hilo Alex Mouko alisema kuwa wahubiri wanaoajiriwa katika shule za umma wanastahili kuwa na wataalam wa masuala ya elimu.
"Nafikiri kuwa hili suala la kuwachuja wahubiri halitotosha na nadhani kwamba kuajiri walimu wanaomwogopa mungu itakuwa ni jambo zuri," alisema Mouko.