Idara ya usajili wa watu katika eneo la Pwani imewaonya maafisa wa utawala dhidi ya kuwaitisha wakazi hongo ili kuwasaidia kupata vitambulisho vya kitaifa.
Kwenye mkao na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumanne, Msajili mkuu wa watu katika eneo la Pwani, Aggrey Masai, alisema kwamba maafisa wake wamepokea lalama hizo kutoka kwa wakazi na lazima hatua hiyo kusitishwa.
Masai alisema kwamba idara hiyo kamwe haihitaji mwananchi kutoa pesa kwa maafisa wa utawala ili kupata vitambulisho vya kitaifa, na kusema kuwa vyeti hivyo vya kitaifa hutolewa bure kwa wananchi.
Alisema kwamba yeyote atakayepatika akiitisha hongo kutoka kwa wananchi atachukuliwa hatua kali za kisheria ili kuhakikisha kwamba wanakabiliana na swala la ufisadi katika afisi za umma katika eneo la Pwani.
"Wananchi wasikubali kutoa pesa kwa maafisa wa utawala kwa sababu vitambulisho hutolewa bure. Machifu watakao patikana wakiitisha hongo kutoka kwa wakazi watakabiliwa kisheria,” alisema Masai.
Kauli ya afisa huyo imejiri baada ya wakazi wa eneo hili kulalakia kukosa vyeti vya kitaifa kufuatia kuitishwa pesa na maafisa wa utawala.