Mratibu katika eneo la Pwani Nelson Marwa amewalaumu maafisa wa uchukuzi na idara ya kukadiria ubora wa bidhaa nchini KEBS kwa kile alichokitaja kama kuzembea kazini.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Marwa alipendekeza maafisa hao kuchunguzwa kufuatia visa vya mara kwa mara vya mali ghushi kunaswa mjini humo, licha ya wao kutikwa jukumu la kuhakikisha uhalali wa bidhaa zinazoingizwa nchini.
“Kuna mtu analala kazini. Itakuaje kila mara bidhaa ghushi zinanaswa hapa Mombasa ilhali kuna mtu aliyepewa mamlaka ya kuzuia mambo kama haya?” aliuliza Marwa.
Aidha, Marwa alidai kuwa maafisa hao huenda wanapokea hongo kutoka kwa wafanyibiashara wanaosafirisha bidha hizo nchini, ili kuwaruhusu kuiendeleza biashara hiyo haramu.
Siku ya Jumatano maafisa wa polisi mjini Mombasa waliyanasa magunia ya mchele yalioingizwa humu nchini kutoka milki za Kiarabu.
Nafaka hizo zilikua zimepakiwa upya katika mifuko mingine ili kuuzwa.
Marwa alisema ataitembelea bohari na hifadhi za nafaka mjini Mombasa, ili kukagua na kubaini uhalali wa bidhaa zinazohifadhiwa humo.