Share news tips with us here at Hivisasa

Mshirikishi mkuu wa utawala kanda ya Pwani Nelson Marwa amemtaka Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kukoma kumdhalilisha naibu wake Hazel Katana.

Hii ni baada ya Katana kutimuliwa ofisini mwake na maafisa wa kaunti hiyo siku chache zilizopita kutokana na madai kuwa anaunga mkono mrengo wa Jubilee.

Kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya idara ya usalama eneo la Pwani mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Marwa alisema kuwa hatua iliyochukuliwa na maafisa wa serikali ya kaunti hiyo ya kumfurusha afisini mwake ni ukuikaji mkubwa wa haki na sheria za nchi.

Marwa alisema kuwa naibu gavana huyo hana uhasama na kiongozi yeyote na iwapo ametangaza kuwania ugavana wakati wa uchaguzi mkuu mwaka wa 2017, ni haki kidemokrasia na kamwe Gavana Joho hafai kumdhalilisha.

“Hatua ya kufurushwa kwa Naibu Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hazel Katana kutoka afisi yake ni ukandamizaji na maafisa wa serikali hiyo wanafaa kuchukuliwa hatua kwani kiongozi huyo hana uhasama na mtu yoyote. Kama amejitenga na Mrengo wa Cord na kuunga mrengo wa Jubilee hiyo ni demokrasia,” alisema Marwa.

Kufurushwa kwa Naibu Gavana wa kaunti ya Mombasa Hazel Katana katika afisi yake pamoja na kutishiwa kupokonywa gari lake na maafisa wa serikali ya Kaunti ya Mombasa kumejiri baada ya Hazel Katana kushughudiwa akihutubia mkutano wa kisiasa mjini Malindi wa mrengo wa Jubilee.