Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amekemewa na vijana katika kaunti ya Nakuru, wakisema matamshi aliyotoa Alhamisi katika hafla moja ya kitamaduni ya Butsoso, eneo la Ematia Navakholo kaunti ya Kakamega, yanaashiria ukabila na ni hatari kwa taifa.
Caro Wairimu kutoka Mirera Naivasha, amesema kwamba Khalwale anafaa kujiepusha na siasa za ukabila zinazosababisha uchochezi wa jamii moja dhidi ya nyingine, ili kuzuia yaliyoipata Kenya mwaka wa 2007 baada ya uchaguzi.
“Hapa Naivasha tulipitia kipindi kigumu sana watu wakipigana na kutofautiana hadharani. Kenya si ya jamii moja, kwa hivyo seneta huyo (Khalwale) azungumze kama kiongozi mkenya sio kama kiongozi wa waluhya,” Wairimu alisema.
Kiongozi wa vijana eneo la Subukia Elijah Murage, alitoa wito kwa wanasiasa kuendeleza siasa zenye lengo la kuunganisha Wakenya kabla ya uchaguzi mwaka wa 2017.
“Siasa za kugawanya wakenya kikabila, kwamba huyu ni Mkikuyu, huyu ni Mkalenjin, yule ni Mluhya na huyu ni Mluo, hazina nafasi katika Kenya ya sasa. Tunachotaka ni kazi kwa vijana, maendeleo na tiba kwa wote wala si mabishano yakujitafutia umaarufu,” Murage alisema.